KABLA SIJAMJUA YESU
Karibuni kwenye ushuhuda wa
mpendwa wetu
Mimi ni mwanamke wa miaka 30.
Ningependa kushiriki na nyie katika ushuhuda wa maisha yangu. Kabla sijamjua
Yesu maisha yangu yalikua yamevurugika. Hakuna kitu nlichokua nafanya
kinafanikiwa. Lakini nikifikiria sasa
naona Mungu alikua ananipenda sana. Kuna mambo mengine nilipita kwa uwezo wake
bila mimi kujua.
Nilibahatika kusoma na kumaliza
chuo. Wakati wenzangu wanahangaika na kazi mimi nilipata tu baada ya kumaliza
chuo. Nilibahatika kupata kazi nzuri yenye mshahara mzuri. Lakini kwa sababu
nisizozielewa baada ya mwaka mmoja tu nikaacha kazi. Nikakosa hamu ya kuendelea
na kazi, nikaondoka huku sijui pa kuanzia.
Pamoja na kwamba nilikua Napata
kipato kizuri kwenye kazi lakini niligundua kwenye mwaka mmoja nliofanya kazi,
sikufanya kitu chochote cha maendeleo. Nililipa kodi, kuvaa na kula. Nikikaa
miezi tisa nyumbani bila kazi, watu wengi walinicheka, nimeacha kazi bila
kupata kazi.
Wakati huo nilikua na boyfriend
ambaye alikua anakuja kwangu kila weekend. Lakini alikua hanisaidii chochote.
Ilikua kama mkosi maana hata yeye alikua anapata kipato kizuri lakini hela yote
inaisha bila kujua matumizi yake. Ikifika tarehe za katikati ya mwezi wote
hatuna kitu!
Hapo ndipo nlipomwona Mungu
akifungua maisha yangu. Kwa sababu nlikua nakaa nyumbani muda wote nilianza kupata hamu ya kumjua Yesu. Nikaanza
kusikiliza mahubiri mbalimbali, nikaanza kusoma Biblia. Siku nzima nakaa ndani
nikisoma na kusikiliza. Nilipata hamu ya kumjua Yesu kiundani na jinsi
anavyofanya kazi.
Siku moja niliambiwa na rafiki
yangu anayefanya kazi kwenye kampuni moja kuna kazi zimetangazwa kwenye kampuni
yao, kwahiyo niombe. Kwavile ana nafasi kubwa angenisaidia. Niliomba nikaitwa
kwenye usaili. Tulikua wengi sana. Tuliambiwa tukusanye vyeti vyetu halali. Cha
ajabu nilikua sijabeba cheti kimoja cha chuo. Nilishangaa nimekisahau vipi. Na
nyumbani ni mkoa tofauti. Nilijipa moyo kuwa haitakua shida sana maana vyeti
vingine vyote nnavyo.
Ilipofika zamu yangu, niliingia,
kitu cha kwanza wanaangalia vyeti. Walipoona sina cheti kimoja waliniambia
hawawezi kunifanyia interview na kwamba niondoke. Huwezi amini nilivyojisikia.
Nililia sana, nilirudi nyumbani siku iliofuata huku nikilia sana nikimlalamikia
Mungu kwa nini ameacha nikaaibika vile.
Niliendelea kukaa nyumbani huku
nikiendelea kusoma na kuomba. Nilikuja
kugundua boyfriend wangu ana wanawake wengi tofauti. Nilipomwuliza tuligombana
sana, akakataa. Nilikubali, lakini moyoni nilikua najua sitakiwi kuwa nae,
tunaishi maisha ya dhambi, ila kwa sababu nilizokua sijui nilikua nashindwa
kufanya maamuzi.
Ilibidi nianze kuishi pamoja na
yule mwanaume kwa sababu kodi yangu iliisha na bado sikua na kazi. Nilikubali
huku nikijua nafanya kosa, nilijua moyoni kua nipo kifungoni, hakua na mpango
na ndoa, nilijua hilo, lakini bado niliendelea kukaa. Sasa hivi najua jinsi
adui alivyokua amedhamiria kuniangamiza, kwa sababu nilikua na uwezo wa kwenda
kuishi kwa mama yangu, japo maisha yake hayakua mazuri sana lakini nyumbani ni
nyumbani. Lakini nilichagua kuishi nae.
Nilijua ni kosa.
Tuliishi huku akionyesha tabia
yake dhahiri, alininyanyasa sana, alikua ana kauli mbaya na wanawake ambao
wengine niliwafahamu kabisa. Wengine walikuja nyumbani. Nilivumilia sana. Kila
siku ilikua mateso kwangu.
Siku moja nikiwa peke yangu
nyumbani nilimwambia Mungu sasa basi. Nimefika mwisho. Najua unanisikia, na
unayaona mateso yangu. Naomba unitoe kwenye kifungo hiki. Nililia sana siku
hiyo, sikuweza kula, nilimwambia Mungu kama wewe ni Mfalme, unaona mateso
yangu, naomba unitoe.
Baada ya siku mbili, akaja rafiki
yetu mmoja nyumbani akasema kwenye shirika anapofanyia kazi kuna kazi
imetanganzwa niombe. Hakua na njia ya kunisaidia Zaidi ya kunipa taarifa hizo
kwani alikua mfanyakazi wa chini kabisa. Niliomba kazi ile hadi saa 6 usiku kwa
sababu deadline ilikua siku hiyo hiyo.
Kesho yake mchana nilipigiwa
simu, nikaambiwa nimefanikiwa kupita
natakiwa kwenye interview! Kazi hiyo ilikua mkoa tofauti na nilipokua naishi na
yule mwanaume. Nilifurahi sana. Nilijiandaa kwenda kwenye interview baada ya
wiki moja. Nilipigiwa simu kesho yake kuwa nimepata kazi!
Nilijua moja kwa moja ni Mungu
amejibu maombi yangu. Moja ya kupata kazi, na nyingine ameniweka mbali na
mwanaume ambae alikua hanifai.
Sasa nimeolewa na mume
anayenipenda na mcha Mungu, naendelea na kazi na namshukuru Mungu kwa kunitoa
kwenye utumwa na kuniweka huru. Nimeweza kumsaidia mama yangu, kumjengea nyumba
na kumwanzishia biashara. Mungu asingejifunua kwangu wakati ule labda ningekua
naendelea na mateso na mwanaume yule, sijui ningekua wapi leo.
Namrudishia Mungu sifa na utukufu
na sitamwacha kamwe.
Asante sana kwa ushuhuda na Mungu aendelee kukubariki sana
ReplyDelete