Tuesday, 18 July 2017

Jinsi ya kupanga ratiba yako ya kila siku ili ufanye yote kwa msaada wa Mungu

Bwana Yesu asifiwe wapendwa.
Katika safari ya mafanikio tunakumbana na mambo mengi. Wakati mwingine kazi zinakua nyingi au masomo yanakua magumu muda wote tunakimbizana. Yote hii ni kufanikisha maendeleo binafsi (personal development).

Katika hali ya kawaida tukifikiria kufanikiwa tunafikiria maisha mazuri, nyumba,  familia nzuri unayoweza kuitimizia kila kitu,, magari, kua na uchumi imara, yaani kutopungukiwa na kitu. Tuna maono mengi na tunajaribu kwa nguvu zetu zote kufanya kazi kwa bidii ili tuyafikie.

Lakini katika yote hayo, nafasi ya Bwana wetu Yesu ipo? Inawezekana ipo, jumapili unahudhuria ibada na bible study. Lakini je inatosha.

Katika shughuli zetu inapaswa kumuangalia Mungu kwanza, halafu uone kupitia yeye (see through Him). Asubuhi hii unapoanza kazi/biashara/masomo yako, muangalie kwanza Mungu, tambua ukuu wake, tafakari jinsi alivyokufanyia mambo mengi, na alivyo msaada kwa kila unachofanya.

Kisha anza kazi yako. Kwenye kila changamoto unayokutana nayo leo, mkumbushe ahadi zake, amesema ukimwomba kitu kwa imani atakupa, amesema hatakuacha.. endelea na kazi yako huku nafsi yako ikiwa imejazwa uwepo wa Mungu.

Unawezaje kufanya hivyo?



Roho Mtakatifu.
“Kadhalika Roho naye hutusaidia udhaifu wetu, kwa maana hatujui kuomba jinsi itupasavyo, lakini Roho mwenyewe hutuombea kwa kuugua kusikoweza kutamkwa.” Warumi 8:26
Roho Mtakatifu hutusaidia mambo mengi sana, kutufundisha, kutukumbusha na la muhimu zaidi hutuombea. Pale unaposhindwa kuomba, ukimtegemea Roho, atakusaidia kufikisha ujumbe kwa Mungu. Hii ndio maana halisi ya Roho kutuombea.
Kwahiyo, katika kila unalofanya, mweke Mungu wa kwanza, kisha uone kupitia yeye. Kama unashindwa kuomba mshirikishe Roho akusaidie, ni msaidizi wetu.

Jinsi ya kupanga ratiba yako.
Haimaanishi uache kazi zote uhudhurie ibada na kufanya maombi. Mungu anaangalia zaidi ndani yako, jinsi nafsi yako inavyomhitaji. Kwahiyo hata katika shughuli zako unaweza kumweka Mungu wa kwanza huku ukiendelea na kazi zako.  Hebu tuangalie kiuhalisia kidogo. Huu ni mfano tu jinsi unavyoweza kufanya.
  1. Tafuta muda asubuhi. Kabla hujaanza kujianda kwenda kwenye shughuli zako, tumia hata dk 10 kwa maombi na kutafakari neno lake. Tafuta mstari wa kutafakari, uandike kwenye dairy au kwenye simu yako.Mfano umechagua  Warumi 8:31 “Basi, tuseme nini juu ya hayo? Mungu akiwapo upande wetu, ni nani aliye juu yetu?”

  2. Ukifika kazini kabla hujaanza kazi mwambie Mungu asante kwa kukuweka pale, kisha tumia hata dk 5 kutafakari mstari uliochagua. Mungu akiwa upande wako hakuna yoyote au chochote kilicho juu yako. Unaweza kufanya yote kwakua yeye anakutia nguvu. Endelea na kazi yako huku ukitafakari kichwani kuhusu ukuu wa Mungu
  3. Kabla ya kutoka kazini, tumia dk chache kumshukuru Mungu na endelea kutafakari jinsi ambavyo wewe ni mwenye nguvu, kama Mungu akiwa upande wako.
  4. Usiku kabla hujalala, tumia dakika chache kuendelea kutafakari huku ukimwambia Mungu asante kwa ulinzi wake.
Unaweza kufanya hivi kimya kimya, bila mtu kujua. Kama unaweza fungulia mahubiri au nyimbo za injili kwenye ili uendelee kutafakari kwa namna hiyo.

Ukiendelea hivyo, ile ahadi ya Mungu inakua ya kwako, anaona ulivyo na moyo wa kumtegemea na anakupa ulichomwomba au hata kizuri zaidi.

Matokeo ya kupanga ratiba yako kwa kumuweka Mungu kwanza:
  1. Kwa uhakika utaona matokeo. Hakuna mtu aliyemtegemea Mungu kwa moyo asione matokeo. Kama huoni matokeo sasa, Mungu anakuandaa kwa kilicho bora zaidi. Usikate tamaa. Endelea kumkumbusha na kutafakari ahadi zake.
  2. Ni njia ya kumshinda shetani. Shetani na watu wasiokutakia mema humkimbia mtu ambae maisha yake yamejaa uwepo wa Mungu. Ataendelea kujaribu kama kuna mwanya kwa sababu ndivyo alivyo, lakini na wewe endelea kukaza kushikilia neno kwa moyo na imani. Hatakuweza. Ataona unavyosonga mbele na unavyofanikiwa kila siku na ukipita mitego yote aliyokuwekea.

  1. Utaishi kwa furaha. Utajishangaa pamoja na matatizo uliyo nayo unakua na amani muda wote. Bwana wetu ni mfalme wa amani. Isaya 26:3, “Utamlinda yeye ambaye moyo wake umekutegemea Katika amani kamilifu, kwa kuwa anakutumaini.”
Mungu ataulinda moyo wako, atakupa amani kamilifu ukimtegemea.

Unaweza ukaamua usipange ratiba yako hivyo. Usimtafute Yesu kwa bidii, usimkumbushe ahadi zake,  usiombe, usitafakari neno.. na bado ukafanikiwa.
Kuna watu wengi wanaotuzunguka waliofanikiwa pengine kuliko sisi na hawamtafuti Mungu wala hawajampa Yesu maisha. Inawezekana kuishi bila Yesu mioyoni mwetu na tukafanikiwa.
Hii ni kwa sababu Mungu ametupa kuchagua, hajamlazimisha mtu kumfuata,unaweza kutegemea akili zako wenyewe, ukiamua usimpe Yesu maisha yako na ukaishi, wala hakuna mtu mwenye haki ya kukuhukumu.
Lakini utaishi hivi kwa neema ya Yesu aliyotupa alivyotoa maisha yake pale msalabani. Unaweza usijue hili, lakini Mungu anakulinda kuliko unavyodhani. Anakupitisha katika hatari nyingi sana.

Tofauti iliyopo kati ya aliyempa Yesu maisha na ambaye bado ni kubwa sana.
Kama humtegemei Yesu, maisha yako hayatakua kamili. Unaweza ukawa unakumbana na matatizo mengi ambayo kama ungemwamini Yesu usingekumbana nayo. Saa zote utakua mtu wa kufadhaika na wasiwasi kwa sababu moyo wako umekosa jambo muhimu.

Lakini ukiamua kumwamini na kumtegemea Yesu,una neema sana. Utashangaa mambo yanakua mepesi na safari ya mafanikio inakua rahisi. Bwana Yesu ni mfalme wa amani. Utakua na amani na furaha kwa kila unachofanya na utakua na mwongozo mzuri wa maisha Yesu akiwa ndani yako na wewe ndani yake.

Katika kuyatafuta mafanikio, ni bora kumuweka Mungu katikati ya kila tunachofanya, ili atuongoze pande zote. Badala ya kujaribu kuzitegemea akili zetu wenyewe, kwani tutashindwa. Mithali 3:5, Mtumaini BWANA kwa moyo wako wote, Wala usizitegemee akili zako mwenyewe.

Haimaanishi usitumie akili, lakini itumie akili yako, huku imani yako na focus yako ikiwa kwa Yesu kwanza. Yeye ndiye aiongoze akili yako, akuoe hekima na maarifa ya kufanya mambo. Mwamini yeye huku ukiendelea kufanya kazi yako kwa bidii. Mshirikishe katika kila unalofanya ili upate mwongozo wake.

Unapoamka mkabidhi njia zako na ukiwa kazini endelea kuomba Roho Mtakatifu akuongoze na kukufundisha. Mshukuru wakati wote hata kama mambo hayaendi vizuri. Na umwombe akutatulie matatizo hayo. Bwana wetu ni mwaminifu sana hatakuacha.

Tukimtegemea Mungu, hata kazi au biashara zetu ziwe changamoto kiasi gani, utashangaa unafanikiwa na saa nyingine utajiuliza umepitaje. Lakini sifa na utukufu zitarudi kwake yeye aliye mkuu sana.

Bwana Yesu akubariki sana!

No comments:

Post a Comment