Karibu tujifunze pamoja
Mara nyingi tunapopata shida tunasahau mema yote Mungu aliyotufanyia. Na baada ya kupita shida hua tunasahau jinsi Mungu alivyotupitisha. Ni udhaifu tulio nao.
Tuangalie mfalme Daudi alivyofanya katika 2 Samweli 22. Daudi baada ya kushinda vita ya wafilisti, alimsifu Mungu na kuelezea jinsi alivyomwokoa. Huu ni mfano mmoja tu kati ya mingi ya mfalme Daudi akiabudu na kusifu baada ya kushinda.
Katika neno hili Daudi amemwelezea Mungu kwa kutumia vitu vyenye nguvu. Mfano, Bwana ni jabali langu, ngome yangu,mwokozi wangu,mwamba wangu, ngao yangu nk. Angalia alivyojimilikisha ukuu wa Mungu. Kila wasifu aliompa Mungu aliufanya wake kwa kusema “yangu”, “wangu”. (Ngome yangu, mwokozi wangu..)
Mfalme Daudi hakujali alipitia mangapi, alichojali wakati huo ni jinsi Mungu alivyomwokoa. Ni dhahiri alikua akiongea maneno hayo akiwa mwenye furaha. Na alikua ameamini kabisa kuwa Mungu ndiye aliyefanya, akaona anastahili sifa zote alizompa.
Katika maisha yetu ni muhimu tujue jinsi ya kumiliki ukuu wa Mungu. Ukijua Mungu ndiye anaekuongoza na kukupa vyote ulivyo navyo, imani yako haitapungua hata wakati wa majaribu.
Ni kawaida kwetu kujiuliza maswali na kumlalamikia Mungu tukihisi amenyamaza. Lakini ukishajihakikishia na kuamini Mungu ndie amekufikisha ulipo, hutaona amekuacha unapopitia shida. Hii ndio maana ya kuufanya ukuu wa Mungu ngao yako.
Tunawezaje kuumiliki ukuu wa Mungu?
- Jifunze kusifu. Kusifu sio kwa mapambio na nyimbo tu. Mstari wa 2-4 Daudi anamsifu Mungu kwa kumpa majina makuu. Na mstari wa nne anasema Mungu ndiye anayestahili kusifiwa. Sura nzima Daudi anamsifu Mungu. Anaelezea jinsi Mungu alivyofanya mambo makubwa na ya kutisha. Unaweza kumsifu Mungu kwa kuongea kama Daudi. Ongea ukuu wa Mungu kwakua ni baba yetu. Elezea jinsi alivyokuokoa na ifanye kama nguzo ya imani yako. Hata kama huna wa kumwelezea, jielezee mwenyewe. Adui asikie jinsi unavyojiamini.
- Tujifunze kukumbuka ukuu wa Mungu. Watu wote ni wadhaifu. Pale tunapopitia shida ndio tunamkumbuka Mungu zaidi. Na pale shida inapopita tunamsahau. Na Mungu anajua hilo na ni jambo analotegema litokee kwa sababu anaujua udhaifu wetu. Lakini, Roho pia hutuongoza na kutukumbusha. Omba Roho mtakatifu akuongoze katika sifa. Akukumbushe ukuu wa Mungu na mambo makuu aliyokufanyia. Hata kama ni miaka kadhaa iliyopita, ukikumbuka leo unasema yes, Mungu alinipitisha pale, na sifa zote zirudi kwake.
- Tumia vitu vinavyokuzunguka kumsifu Mungu. Najua wengi tunafanya lakini labda tuongeze zaidi. Mfano, Kuweka nyimbo za sifa, tumia simu yako kusave kumbukumbu ya mambo makuu Mungu aliyokufanyia, andika kwenye diary, ukiwa njiani sikiliza mahubiri nk. Nyumba yako, ofisi yako, gari yako, simu yako, tablet, laptop, zote zijae sifa. Kama vile mtu mwingine anavyoweza kuamua kuweka na kuangalia movie au muziki kwenye kila device aliyo nayo, na wewe amua kuweka sifa za Mungu. Hii itakusaidia kuwa kwenye uwepo wa Mungu wakati wote.
Faida za kumiliki ukuu wa Mungu
- Unamwonyesha Mungu kua unamwamini. Ni mara ngapi tumekua tukihitaji msaada kwa baba zetu?. Umewahi kukaa na watu wakiwasifia wazazi wao, mzee kanitafutia chuo, biashara, kiwanja, kazi, nk. (Wakati mwingine hata mwenza) Kwanini watu wanapenda kuwaambia wengine waliyofanyiwa na wazazi. Ni kwa sababu wanajisikia fahari. Jisikie fahari (proud) pia Mungu anapokufanyia jambo na uliseme na kumsifia. Mungu anapenda tumwamini, ndio maana tumeokolewa kwa imani. Kwahiyo moja wapo ya njia ya kumwonyesha Mungu unamwamini ni kuumiliki ule ukuu wake kwa kumsifu.
- Inatusaidia pale tunapopata jaribu lingine. Ukimiliki sifa na ukuu wa Mungu ni akiba, vitakusaidia kupita katika jaribu lingine. Kumbuka majaribu yapo, na yatakuja, ni njia ya kupima imani yetu. Ukiwa katikati ya jaribu, huku unamsifu Mungu na kuusema ule ukuu wake, vitakusaidia kua na moyo imara. Hutaishi kwa hofu, bali utakua na furaha kwa sababu unajua Mungu alivyo mwamba na mwokozi wako, ni lazima atakupa ushindi.
- Adui anatambua kua unajielewa. Hakuna kitu kinachomchanganya adui kama kuona unajielewa. Shetani anapoleta majaribu tumaini lake ni kukuangusha. Anakata tamaa anapoona tunaishi ndani ya Mungu na tunajua alivyo mkuu. Tunashinda majaribu kwa njia hiyo. Ni muhimu kumwonyesha adui kua huogopeshwi na tatizo, bali unafurahishwa na ukuu wa Mungu na una imani kwa Mungu kua atakuokoa na kukutoa kwenye tatizo hilo.
Mungu ni mkuu sana, kila kitu kinachotuzunguka kinashuhudia ukuu wake. Hata kama umeomba kitu fulani kwa Muda mrefu na hujapata, angalia kile alichokufanyia(lazima kipo) na umwambie unajua jinsi alivyo muweza na alikufanyia kitu fulani. Unajua kabisa hata hicho unachoomba atafanya. Endelea kumkumbusha kila siku. Mungu wetu tayari anajua mahitaji na shida zetu zote. Anachotaka ni imani zetu. Mkumbushe na amini kuan atafanya. Usiwe na wasiwasi moyoni. Jiamini na mwamini Mungu alipokutoa ni mbali, na unapoelekea ataendelea kua pamoja na wewe. Alishasema hatakuacha wala kukupungukia kamwe. Amen
No comments:
Post a Comment