Wednesday, 12 July 2017

Jinsi ya kuulinda moyo wako usiumizwe

Wote tunajua kuumizwa moyo katika mahusiano. Kwa namna moja au nyingine kila mtu ameumizwa na na mtu mwengine,  kwenye mahusiano mbalimbali, kama urafiki, ndoa, kazi, biashara nk.  Unapofanyiwa jambo baya kwenye uhusiano moyo unaumia. Kuna hisia unapata ya moyo kukosa amani, kuuma, kuwa na wasiwasi na kukosa kujiamini.  Unaweza ukaumia kwa muda na baadae unapoa.
Kwa nini tunaumia?
Ni pale unapotegemea kupata vitu fulani kwa mwenzako (mume, mke, mchumba,rafiki, mzazi nk), halafu unapata kinyume na ulivyotegemea. Au anakufanyia jambo baya ambalo hukutegemea. Mfano, mke au mume anakua na uhusiano nje ya ndoa. Ukijua lazima itauma sana. Au rafiki anakusaliti, au kukudhulumu, lazima moyo unakuuma kwa sababu ni kinyume na ulivyotegemea.

Kwa nini tunategemea mambo mazuri kutoka kwa wenzetu?
Ni kwa sababu tumejenga uaminifu kwao. Unamwamini mume au mke wako sana kwa hiyo unaamini hataweza kukufanyia jambo baya. Pia ni kwa sababu ya ukaribu tulio nao kwao. Una rafiki wa karibu sana mnajuana na kutunziana siri, unajua kwa ukaribu mlio nao hawezi kukuumiza.

Ni nini hua kinabadilika?

Binadamu. Sisi wote ni wadhaifu. Dunia imejaa kila aina ya vishawishi na tamaa zimetujaa. Ni rahisi kumsaliti mtu wako wa karibu kuuridhisha moyo wako. Pia adui kama ilivyo asili yake ya udanganyifu, hutudanganya tufanye jambo kwa ubinafsi bila kujali tunawaumiza wenzetu.  Lakini kila kitu hua kinabadilika mwenzako akijua ulichofanya. Wewe unaweza kubaki unajilaumu na kuomba msamaha lakini yeye anaanza kuumia na kujiuliza maswali mengi bila majibu.

Madhara ya kuumizwa ni mengi: magonjwa ya moyo, kurudi nyuma kimaendeleo kwa sababu ya kutumia muda mwingi kuwaza, kupoteza kazi, masomo, kupoteza mwelekeo wa maisha (kupoteza malengo yako), kupata mawazo mabaya kama kujiua, kupoteza vitu vya thamani, na muhimu zaidi kupoteza watu muhimu maishani mwako kama watoto nk.

Lakini kuna habari njema. Unaweza kuepuka kuumizwa moyo wako.
Unawezaje?
  1. Acha kuwekeza moyo wako kwa watu. Yeremia 17:9  inasema “Moyo huwa mdanganyifu kuliko vitu vyote, una ugonjwa wa kufisha; nani awezaye kuujua?” Moyo unaweza ukakudanganya ukadhani hapo ulipo ni salama kumbe sio. Na hakuna anayejua moyo, bali ni Mungu pekee. Kwahiyo ili uwe salama, usiwekeze moyo wako wote kwa watu, ukaona bila mtu fulani siwezi kuishi, siwezi kua na furaha. Weka moyo wako kwa Mungu kwanza, ndio watu wengine wafuate.  Luka 10:27 inasema “Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa nguvu zako zote, na kwa akili zako zote; na jirani yako kama nafsi yako” Unaanza kumpenda Bwana Mungu wako Kwanza, ndipo watu wafuate. Hata katika ndoa, Kristo awe wa kwanza, ndipo mke/mume afuate. Mungu alipokuumba alikua na malengo na wewe, alishakuwekea misingi kabla hujazaliwa. Kwahiyo usifikiri bila mtu fulani mimi sio kitu, ukavumilia kuumizwa. Kwa jinsi Mungu anavyotupenda, ukimtegemea anakuonyesha watu wema aliokuandalia, wa kukusaidia kwenye malengo yako. Usivumilie mtu anayekutenda vibaya kwa kudhani Mungu ndio alivyopanga. Labda uwe na uhakika kweli 100% Mungu amepanga upite hapo. Vinginevyo mwombe akupe watu wema wenye upendo wa kweli na mtu ambaye mtaendana ili akusaidie kuishi kwa misingi Mungu aliyokuwekea. Mfano, kama Mungu amepanga uwe mwalimu, daktari, mpishi, basi mtu huyo akusapoti kutimiza hayo.

  1. Wekeza moyo wako kwa Mungu.  Zaburi 51:10, “Ee Mungu, uniumbie moyo safi,uifanye upya roho iliyotulia ndani yangu” Omba Mungu akupe moyo safi na roho iliyotulia. Ukiwa unaingia kwenye mahusiano mapya, uwe na moyo safi ili moyo huo usikudanganye. Mithali 4:23 inatukumbusha kulinda mioyo yetu, maana ndipo zitokazo chemchemi za uzima. Moyo ukiwa safi unapata uzima wa maisha ya hapa na unategemea kupata uzima wa milele, kwa sababu Yesu ameutawala moyo wako.

  1. Omba akili, hekima na maarifa. Ukweli ni kwamba kwa nguvu zetu hatuwezi kujua ni mtu yupi mwenye nia mbaya. Hasa kwenye mahusiano ya kuelekea kwenye ndoa. Unaweza ukaweka moyo wako wote kwa mtu kumbe yeye hana mpango kabisa. Mpaka uje kutambua unakua umeshaumia sana, na umepoteza muda mwingi na mambo mengine muhimu. Mungu ndie atupae hekima na maarifa ya kutambua mambo. Omba Roho Mtakatifu akuongoze katika uhusiano huo. Atakuonyesha mwanzo kabisa kama upo sahihi au la. Na ukionyeshwa, uwe tayari kutii. Usilazimishe jambo ambalo moyo wako unaoongozwa na Roho unakuambia hapana.

  1. Usilazimishe. Kama nilivyosema hapo juu, usilazimishe mambo. Kama unaona uhusiano hauendi vizuri, na kila unapoomba Mungu anakuonyesha hivyo ni bora kutii. Usipofanya hivyo unajitafutia kuendelea kuumia. Hii ni hasa kwa mahusiano yanayoelekea ndoa. Ni muhimu kuomba sana, ili uwe na uhakika kwenye kila hatua.

Kwa maelezo hayo, haina maana tusiwapende watu. Tumeambiwa katika Luka 10:27 tuwapende jirani zetu kama nafsi zetu. Upendo kati yetu ni muhimu sana.
Lakini pale unaposalitiwa na kuumizwa, kuwa makini  kwenye hatua inayofuata. Usikubali kuendelea kuumizwa. Una thamani kubwa na una moyo safi, lakini inawezekana unayetaka kuanzisha naye mahusiano hayupo hivyo. Kila mtu ana moyo wa tofauti. Inategemea amewekaje uhusiano wake na Mungu.  Kwahiyo hatua muhimu ni kumuomba Bwana Yesu akuonyeshe na kukuongoza katika kila hatua ya uhusiano.
Kama unaamini Mungu amebariki, basi  endelea kumuweka Mungu wa kwanza kwenye uhusiano huo, na wengine au mwenza wako afuate.

Tumaini kubwa sana tulilo nalo ni kwa Mungu. Kwa sababu hulinda mioyo yetu. Isaya 26:3 “Utamlinda yeye ambaye moyo wake umekutegemea Katika amani kamilifu, kwa kuwa anakutumaini.” Ukimtegemea Mungu ataulinda moyo wako na utajua mapema kabisa kabla ya kujiingiza kwenye uhusiano hatarishi.

Tumaini lingine kubwa, jinsi Mungu wetu anavyotupenda, hata ikitokea moyo ukadanganyika na kuumia, yeye huuganga. Zaburi 147:3  “Huwaponya waliopondeka moyo, Na kuziganga jeraha zao”. Kwahiyo kama umeumizwa moyo, mwambie Mungu akugange. Ameshaahidi kwahiyo wewe mdai kwa nidhamu na utii ili akupatie.

Sala: Mungu tunaomba utuumbie mioyo safi na utuongoze tunapoingia kwenye mahusiano, uyabariki ili tuweze kuishi ndani ya haki yako. Tunaomba utugange mioyo yetu iliyopondeka iwe mipya na kuanzia sasa tuweze kukuweka wewe kwanza mioyoni mwetu, na watu wengine wafuate. Utuondolee ubinafsi wa kujipenda wenyewe kuliko jirani zetu, na utubariki ili tuwabarikie wengine. Amen.

No comments:

Post a Comment