Friday, 15 September 2017

Ushuhuda-Kabla sijamjua Yesu


KABLA SIJAMJUA YESU

Karibuni kwenye ushuhuda wa mpendwa wetu

Mimi ni mwanamke wa miaka 30. Ningependa kushiriki na nyie katika ushuhuda wa maisha yangu. Kabla sijamjua Yesu maisha yangu yalikua yamevurugika. Hakuna kitu nlichokua nafanya kinafanikiwa.  Lakini nikifikiria sasa naona Mungu alikua ananipenda sana. Kuna mambo mengine nilipita kwa uwezo wake bila mimi kujua.

Nilibahatika kusoma na kumaliza chuo. Wakati wenzangu wanahangaika na kazi mimi nilipata tu baada ya kumaliza chuo. Nilibahatika kupata kazi nzuri yenye mshahara mzuri. Lakini kwa sababu nisizozielewa baada ya mwaka mmoja tu nikaacha kazi. Nikakosa hamu ya kuendelea na kazi, nikaondoka huku sijui pa kuanzia.



Pamoja na kwamba nilikua Napata kipato kizuri kwenye kazi lakini niligundua kwenye mwaka mmoja nliofanya kazi, sikufanya kitu chochote cha maendeleo. Nililipa kodi, kuvaa na kula. Nikikaa miezi tisa nyumbani bila kazi, watu wengi walinicheka, nimeacha kazi bila kupata kazi.

Wakati huo nilikua na boyfriend ambaye alikua anakuja kwangu kila weekend. Lakini alikua hanisaidii chochote. Ilikua kama mkosi maana hata yeye alikua anapata kipato kizuri lakini hela yote inaisha bila kujua matumizi yake. Ikifika tarehe za katikati ya mwezi wote hatuna kitu!




Hapo ndipo nlipomwona Mungu akifungua maisha yangu. Kwa sababu nlikua nakaa nyumbani muda wote  nilianza kupata hamu ya kumjua Yesu. Nikaanza kusikiliza mahubiri mbalimbali, nikaanza kusoma Biblia. Siku nzima nakaa ndani nikisoma na kusikiliza. Nilipata hamu ya kumjua Yesu kiundani na jinsi anavyofanya kazi.

Siku moja niliambiwa na rafiki yangu anayefanya kazi kwenye kampuni moja kuna kazi zimetangazwa kwenye kampuni yao, kwahiyo niombe. Kwavile ana nafasi kubwa angenisaidia. Niliomba nikaitwa kwenye usaili. Tulikua wengi sana. Tuliambiwa tukusanye vyeti vyetu halali. Cha ajabu nilikua sijabeba cheti kimoja cha chuo. Nilishangaa nimekisahau vipi. Na nyumbani ni mkoa tofauti. Nilijipa moyo kuwa haitakua shida sana maana vyeti vingine vyote nnavyo.

Ilipofika zamu yangu, niliingia, kitu cha kwanza wanaangalia vyeti. Walipoona sina cheti kimoja waliniambia hawawezi kunifanyia interview na kwamba niondoke. Huwezi amini nilivyojisikia. Nililia sana, nilirudi nyumbani siku iliofuata huku nikilia sana nikimlalamikia Mungu kwa nini ameacha nikaaibika vile.

Niliendelea kukaa nyumbani huku nikiendelea kusoma na kuomba.  Nilikuja kugundua boyfriend wangu ana wanawake wengi tofauti. Nilipomwuliza tuligombana sana, akakataa. Nilikubali, lakini moyoni nilikua najua sitakiwi kuwa nae, tunaishi maisha ya dhambi, ila kwa sababu nilizokua sijui nilikua nashindwa kufanya maamuzi.

Ilibidi nianze kuishi pamoja na yule mwanaume kwa sababu kodi yangu iliisha na bado sikua na kazi. Nilikubali huku nikijua nafanya kosa, nilijua moyoni kua nipo kifungoni, hakua na mpango na ndoa, nilijua hilo, lakini bado niliendelea kukaa. Sasa hivi najua jinsi adui alivyokua amedhamiria kuniangamiza, kwa sababu nilikua na uwezo wa kwenda kuishi kwa mama yangu, japo maisha yake hayakua mazuri sana lakini nyumbani ni nyumbani.  Lakini nilichagua kuishi nae. Nilijua ni kosa.

Tuliishi huku akionyesha tabia yake dhahiri, alininyanyasa sana, alikua ana kauli mbaya na wanawake ambao wengine niliwafahamu kabisa. Wengine walikuja nyumbani. Nilivumilia sana. Kila siku ilikua mateso kwangu.

Siku moja nikiwa peke yangu nyumbani nilimwambia Mungu sasa basi. Nimefika mwisho. Najua unanisikia, na unayaona mateso yangu. Naomba unitoe kwenye kifungo hiki. Nililia sana siku hiyo, sikuweza kula, nilimwambia Mungu kama wewe ni Mfalme, unaona mateso yangu, naomba unitoe.

Baada ya siku mbili, akaja rafiki yetu mmoja nyumbani akasema kwenye shirika anapofanyia kazi kuna kazi imetanganzwa niombe. Hakua na njia ya kunisaidia Zaidi ya kunipa taarifa hizo kwani alikua mfanyakazi wa chini kabisa. Niliomba kazi ile hadi saa 6 usiku kwa sababu deadline ilikua siku hiyo hiyo.

Kesho yake mchana nilipigiwa simu, nikaambiwa  nimefanikiwa kupita natakiwa kwenye interview! Kazi hiyo ilikua mkoa tofauti na nilipokua naishi na yule mwanaume. Nilifurahi sana. Nilijiandaa kwenda kwenye interview baada ya wiki moja. Nilipigiwa simu kesho yake kuwa nimepata kazi!

Nilijua moja kwa moja ni Mungu amejibu maombi yangu. Moja ya kupata kazi, na nyingine ameniweka mbali na mwanaume ambae alikua hanifai.

Sasa nimeolewa na mume anayenipenda na mcha Mungu, naendelea na kazi na namshukuru Mungu kwa kunitoa kwenye utumwa na kuniweka huru. Nimeweza kumsaidia mama yangu, kumjengea nyumba na kumwanzishia biashara. Mungu asingejifunua kwangu wakati ule labda ningekua naendelea na mateso na mwanaume yule, sijui ningekua wapi leo.



Namrudishia Mungu sifa na utukufu na sitamwacha kamwe. 

1 comment:

  1. Asante sana kwa ushuhuda na Mungu aendelee kukubariki sana

    ReplyDelete