Karibu kwenye somo la pili la Uvumilivu wakati wa kusubiri majibu
Leo tunaendelea na kuangalia tunachotakiwa kufanya wakati tunasubiri Mungu ajibu tulichomwomba. Kumbuka kuna wakati wa kusubiri, sio mara zote Mungu hujibu muda huohuo ulioomba.
Wakati huo wa kusubiri, tuangalie tunaweza kuishi vipi ili majibu yakija yatukute tupo tayari kupokea.
1.
Tuombe
Mungu atupe kustahimili.
Yakobo 1:12 “Heri mtu astahimiliye
majaribu; kwa sababu akiisha kukubaliwa atapokea taji ya uzima, Bwana
aliyowaahidia wampendao”
Wakati wa kusubiri majibu ndio wakati kuna majaribu
mengi. Adui anakupa mikakati na njia za uongo za kutatua tatizo lako. Kama
hujasimama unaweza kuzifuata na utapotea.
Mungu pekee ndiye anaeweza kutupa ustahimili. Roho Mtakatifu ni msaada
wetu. Alikuja duniani ili kutusaidia. Tukimtegemea yeye wakati tunasubiri
tutaweza kustahimili hadi pale Mungu atakapoleta majibu.
2. Omba furaha na Amani. Warumi 5:3-5. Paulo
anatufundisha kufurahi katika dhiki. Kwanini ufurahi? Kwa sababu dhiki huleta
saburi (uvumilivu), na uvumilivu huleta uthabiti wa moyo. Uthabiti ni ule utu
uliojijenga kwako (personality) kutokana na shida uliyopitia. Unakua imara na
kuwa na nguvu ya kukabiliana na jambo.
Moyo wako hautetereki unapopata shida kama hiyo tena,
unakua umemaster kwa jambo hilo, unajua kabisa ukikutana na shida hiyo tena
maishani mwako, moyo wako unaweza kukabiliana kwa sababu ni thabiti (uimara)
uliopata. Uthabiti pia unakuongezea Imani yako kwa Mungu. Una uhakika kabisa
ukiwa na hitaji lingine na ukimwomba Mungu atakutimizia.
Na uthabiti huo
huleta tumaini, una tumaini kabisa kwamba Mungu atakutatulia shida yako,.
Ndiyo sababu tunaambiwa kufurahi wakati wa dhiki.
Ukiweza kupata uvumilivu, uthabiti wa moyo na tumaini, endapo utapata shida
kama hiyo tena tayari unajua njia jinsi ya kuomba na kuamini.
3. Kuwa mtiifu kwa Mungu. Waebrania
10:36, Waebrania 6:12. Wakati unasubiri tafuta sana kuyafanya mapenzi ya Mungu.
Kuwa mtiifu kwa Mungu, fanya matendo mema. Haya yote yanawezekana kama Roho
yupo ndani yako. Roho atakua ndani yako, kama utasoma neno la Mungu. Jitahidi
kukaa uweponi mwake wakati wote unapokua unasubiri Mungu akupe muujiza
wako. Hudhuria maombi, bible study,
tenga muda wa kutosha kuomba, watendee watu mambo mema, toa msaada pale
unapohitajika nk.
Ukiweza
kuyafanya mapenzi ya Mungu kwa uaminifu utaipata ile ahadi (soma Waebrania
10:36). Mungu ni mwaminifu kwetu, ukiwa mtiifu kwake kwa kutenda mapenzi yake,
naye atakutimizia ahadi yake kwako.
4. Epuka dhambi (Waebrania 12:1). Wakati unasubiri
na kuwa na saburi (uvumilivu) epuka kufanya dhambi. Wakati mwingine ni ngumu,
kwa sababu ya miili yetu dhaifu, lakini Bwana ni mwaminifu, hata pale
tunapoanguka dhambini, tukikiri kwa uaminifu anatusamehe. Ili uepuke dhambi
omba Roho Mtakatifu akuongoze kufanya mambo yote kwa mpango wa Mungu. Akupe
matamanio ndani ya moyo wako kufanya yale yanayompendeza Mungu. Mungu anajua tulivyo
na mizigo mizito, ndio maana alimtoa mwanae Yesu Kristo Bwana wetu ili atupe
ondoleo la dhambi.
5. Mwamini Mungu. (Mithali 3:5-6, Warumi 12:16).
Hapa wengi tunapata shida. Kujiuliza kweli Mungu atafanya? Unaomba lakini huna
uhakika Mungu atafanya. Kuna mistari mingi sana kwenye biblia inayotuambia
kumwamini Mungu. Imani yako ndio itakupa majibu unayosubiri. Haimaanishi Mungu
hawezi kufanya usipoamini. Kuna mambo mengi sana Mungu anafanya ambayo hata
hatujui. Kuna hatari nyingi anakukinga hujui. Lakini Mungu anataka umwamini kwa
sababu alituumba ili tumtegemee yeye. Sisi ni watoto wake. Kila baba anapenda
kuaminiwa na mwanae. Ndivyo ilivyo kwa Mungu. Anataka umtegemee na kumwamini
kuwa atakufanyia yale uliyomwomba.
Hakuna jambo linalomfurahisha Mungu kama pale watoto
wake wanapomwamini. Ukiwa na Imani kwa Mungu yote yanawezekana.
Jambo la muhimu ni kudumu kwenye maombi. Katika kuvumilia
kwako, pia kunaambatana na maombi. 1 Thesalonike 5:17: “Ombeni bila kukoma;”
Omba hadi uone mabadiliko.
Unaposubiri majibu ya uliloomba kwake, endelea
kumkumbusha Mungu na kumwonyesha imani yako. Na yeye atakutimizia hitaji lako.
Jaribu leo kufanya haya na utaona majibu ya muujiza uliokua unauongojea.
Tunajaribu kukupa mwongozo wa kujitegemea katika
maombi, ili uweze kusimama mwenyewe na uone matokeo ya maombi yako.
Mungu akubariki.

No comments:
Post a Comment