Bwana Yesu asifiwe wapendwa.
Wengi hua tunatamani kuanzisha biashara au kazi ambazo tunataka kuzisimamia wenyewe. Inaweza kuwa vitu kama ufugaji, kilimo, biashara za bidhaa, vyakula, kuandika vitabu, kufundisha, kuhubiri, salons, magari, kuanzisha kampuni mbalimbali nk. Chochote kile unachotamani kufanya mbali na kazi yako ya kuajiriwa. Naamini ni watu wachache wasio na ndoto za kufanya mambo yao binafsi ya kuingiza vipato.
Faida za kazi/biashara binafsi.
- Kujiridhisha kuwa unaweza kufanya jambo mwenyewe, (personal satisfaction). Inakupa kujiamini unaweza kufanya jambo lako peke yako kwa mafanikio na likakuingizia faida ya kiuchumi na kwa jamii.
- Unajisikia kutimiza karama au kipaji unachoamini umepewa na Mungu. Kama una karama ya kuandika siku ukifanikiwa kutoa kitabu chenye kuleta faida kwa jamii utajisikia furaha kua umetimiza karama uliyopewa.
- Kuleta faida kiuchumi, kipato kuongezeka. Ukifanikiwa kufanya jambo peke yako na ukafanikiwa kupata faida ni furaha sana.
- Kupata mwelekeo mzuri wa maisha. Haimaanishi anayetegemea mshahara peke yake hana mwelekeo, lakini ni jambo kubwa zaidi ukiweza kutumia akili yako kuanzisha kitu na kukisimamia, na kuleta faida na matokeo chanya kwa jamii. Hata waliokuajiri walianza na wazo kama hilo, wakaweza kuendelea hadi kufanikiwa kuajiri.
- Kujiamini. Unajisikiaje kuwa bosi wako mwenyewe? Lazima kuna furaha na kujiamini kuwa umeweza.
Sasa mara nyingine tunapata shida kuanzisha biashara au kazi za kujitegemea. Kwa sababu ya mambo mbali mbali ikiwemo kutokujiamini, adui kufunga milango, aibu, uoga, malezi nk. Hapa chini kuna mwongozo wa mambo ya kufanya kabla ya kuanzisha biashara au kazi ya kujitegemea (self employment).
- Usikubali mtu akuambie kuwa huwezi kufanya jambo fulani kwa sababu Mungu ametupa uwezo wa kufanya jambo lolote kwa nguvu zake. Wafilipi 4:13. Hii ni muhimu kwa kuanzia. Amini kwanza una uwezo wa kufanya jambo lolote la halali unalotaka hapa duniani kwa sababu Mungu amekupa uwezo huo. Hapa issue sio kuamini jambo unalotaka kufanya, msisitizo ni kumwamini Mungu aliyekupa uwezo. Weka imani yako kwake.
- Tafuta karama/kipaji chako. Ili uweze kufanikiwa ni vizuri ujue ni kitu gani unaweza kufanya vizuri sana. Inawezekana unajiamini kwamba unaweza kufanya mambo mengi, lakini ukijaribu unashindwa. Ili ujue unachoweza kufanya mwombe Mungu akuonyeshe. Fanya hivi kwa kuitafuta furaha yako kwa Mungu, ili akupe yale unayotamani kufanya. (Zaburi 37: 3-5.) Maana nyingine ni kwamba yale matamanio yako yawe yametengenezwa na Mungu mwenyewe, na ayafanye ya kwako, ili usifanye jambo kinyume na mapenzi yake. Mfano kama unatamani kufanya biashara, mwombe Mungu akupe matamanio (desire) yake kuhusu biashara anayotaka yeye wewe uifanye. Halafu aifanye iwe ya kwako, ili ufanye exactly kile kitu Mungu anachotaka ufanye. Faida yake ni kwamba atakupa silaha zote za kukabiliana na changamoto za biashara hiyo. Yaani itakua ndani ya uwezo wako. Na pia utaipenda sana. Kwa sababu ni biashara ambayo Mungu alikuwekea matamanio ya kuifanya. Na itakua biashara halali. Imetoka kwa Mungu.
- Mwombe Roho wa Mungu akupe mwongozo. Kisha mwamini Mungu aliekupa uwezo ili athibitishe njia zako. (Mithali 3:5-6). Kabla hujaanza jambo unalotaka, mshirikishe Mungu kuanzia mwanzo. Usisubiri umeona changamoto ndio uanze kumwita. Muweke wa kwanza ili athibitishe kila unalofanya. Kwa njia hii hata changamoto zikija hutakua na uoga, na utaweza kutafuta suluhisho. Msingi wako uwe ni Yesu Kristo. Usikubali kufanya jambo bila kumshirikisha kwanza. Mwambie unataka kufanya jambo fulani kisha lifanye. Kwa uwezo wake atatengeneza njia.
- Ondoa aibu. Ok, aibu ni jambo linalokwamisha sana maendeleo. Kama Mungu amekuonyesha kufanya biashara ya kuuza mkaa, usiangalie nani anasema nini. Mfano mzuri ni Yesu Kristo mwenyewe.
“Tukimtazama Yesu, mwenye kuanzisha na mwenye kutimiza imani yetu; ambaye kwa ajili ya furaha iliyowekwa mbele yake aliustahimili msalaba na kuidharau aibu, naye ameketi mkono wa kuume wa kiti cha enzi cha Mungu. Waebrania 12:2”
Bwana Yesu ni mfano mzuri sana wa kuishinda aibu. Aliangalia furaha iliyokua mbele yake baada ya kumaliza kazi. Alimaliza kazi yake Mungu aliyomtuma kwa ushujaa na sasa ameketi mkono wa kuume wa kiti cha enzi cha Mungu. Fikiria kama angewaza aibu ambayo angeipata ya kupigwa hadharani na kutemewa mate.
Unawezaje kuishinda aibu? Kwanza usijifananishe na mtu yoyote. Tunapenda kurudia kuwa wewe ni wa kipekee hapa duniani, hakuna mtu anayefanana na wewe. Pili, alichopangiwa mwingine sio ulichopangiwa wewe, kwahiyo usifikiri kwa sababu yule ameweza kufanikiwa kwenye biashara ya mgahawa na wewe utafanikiwa. Labda ujue kwa hakika umeitiwa hivyo. Na jambo la tatu, usifikirie aibu utakayopata ukifanya jambo uliloitiwa, kwani utaishia kutokulifanya. Fikiria zaidi faida, na matokeo (impact) jambo ya jambo hilo.
Utajuaje Kama Mungu amekujibu
Utajuaje kama Mungu amejibu ufanye jambo fulani. Kwanza kabisa kama umemwamini kwa moyo wako wote atajibu. Umeomba kwa imani, huna wasiwasi umetulia ukiamini kuwa Mungu atajibu kwa wakati wake, atajibu.
Akishajibu, angalia msukumo unaoupata kufanya jambo hilo. Angalia fursa zinazokuja zinazoendana na jambo hilo. Hapo ujue Mungu amejibu. Wengi huwa tunaangalia mambo makubwa. Mfano unategemea mtu akupe mtaji ndio ujue Mungu amejibu, ndio anaweza kujibu kwa namna hiyo, lakini angalia usipitwe kwa kuangalia mambo makubwa.
Muhimu zaidi angalia ule msukumo wa ndani, matamanio (desire) unayopata kufanya jambo lile, hiyo itakufanya ujiskie kusoma zaidi na kutafiti kuhusu jambo hilo. Ujue hapo ndio Mungu anakuonyesha mwelekeo. Utatamani kila saa kujifunza na kutafuta fursa juu ya jambo hilo. Na ukitafuta utazipata.
Mungu huweka desire ndani yetu kuhusu mambo mbalimbali. Jinsi unavyochukua hatua juu ya jambo ulilowekewa ndio fursa zinavyofunguka zaidi.
Usikubali kubaki nyuma. Roho wa Mungu akuongoze kutambua Mungu anachokuitia.
points za kukumbuka.
- Hufanani na mtu yoyote. Una kipaji/karama/huduma tofauti na mtu mwingine ndani yako, inayoweza kuleta faida kwako na kwa watu wengine. Mwombe Mungu akufunulie ili uanze kuifanyia kazi.
- Unaweza kufanya jambo lolote kwa uwezo wa Mungu. Mshirikishe yeye kabla hujaanza, kama umeshaanza bado hujachelewa, mwombe Mungu aingie katikati ya jambo unalofanya sasa na akupe mwongozo. Utashangaa matokeo yake. Na unaweza kubadili mwelekeo kabisa na ukafaidika zaidi kwa sababu Mungu atakuongoza kwenye mafanikio.
- Usiogope. Hata kama umeshaanza kufanya kazi au biashara mara nyingi ukafeli, usikate tamaa. Bado una nafasi. Huduma ya mtu haizeeki hata mtu akizeeka, ile huduma itaendelea kuonekana tu.
- Sio kila mtu ameitwa kufanya biashara au kazi ya kujitegemea. Yusufu alikua mwajiriwa hadi mwisho. Baada ya kuuzwa kwa waishmaeli alikua mtumwa wao, kisha kwa Potifa, gerezani na baadae kwa Farao. Japo alikua ana mamlaka makubwa sana kwa Potifa na kwa Farao, lakini alikua chini yao. Mungu alimwinua kwenye ajira yake kuwa mtu mkubwa sana. Potifa alikua hajui chochote kuhusu mali zake, alimwachia kila kitu kiwe chini yake, kasoro mke wake. (Mwanzo 39:9) Yusufu alisitawi akiwa ndani ya nyumba ya bosi wake Potifa. (Mwanzo 39:2). Yaani alipata mafanikio makubwa lakini akiwa chini ya bwana wake Potifa.
Hata gerezani Yusufu alikua mkuu wa wafungwa. Wala mkuu wa gereza hakuangalia jambo lolote. Kama Mungu hakukupa kipawa cha kuanzisha biashara, usihuzunike, hapo alipokuweka anakustawisha. Mfano mzuri ni mawaziri, marais na watu wengine wenye vyeo vikubwa, wale wamepandishwa na Mungu, japo bado ni wafanyakazi walio chini ya mamlaka. Mungu amewapa karama ya uongozi na hapo hapo wamestawi.
Ubarikiwe sana. Katika masomo yajayo tutajifunza kujua kama hapo ulipo kwenye kazi, masomo au biashara ni sehemu sahihi.
Mwongozo wa sala:
Bwana Yesu asante kwa baraka zako za kila siku. Naomba unifunulie niweze kujua huduma yangu, na karama uliyoweka ndani yangu. Naomba unionyeshe uwezo wangu ili niweze kuishi kusudi lako uliloweka ndani yangu.
Naomba unionyeshe biashara au kazi unayotaka mimi nifanye, unipe na mpango na vifaa/fursa za kuifanya.
Nakuomba wewe kwa sababu nakuamini, naamini uwezo wako, naamini ukinipa wewe nitafanikiwa, kwa akili zangu ziwezi, bali kwa uwezo wako.
Naokuomba kwa sababu nikijaribu kwa akili zangu nitashindwa. Naomba uupe moyo wangu na akili zangu uwezo wa kutambua jambo utakalonipa.
Amen.
Unaweza kusali sala hii ukiongeza maneno yako kila siku hadi utakapofanikiwa. Nasi tunaomba Roho wa Mungu akuongoze katika kuomba kwako na kutimiza kile ambacho Mungu ataweka ndani yako. Amen
No comments:
Post a Comment