Friday, 7 July 2017

Weekend ya kushukuru: Jinsi ya kumshukuru Mungu wakati wa shida

Karibu kwenye weekend ya kushukuru.

Ni ngumu binadamu kumshukuru Mungu wakati wa matatizo na changamoto. Mara nyingi tunaishia kumlalamikia Mungu na kumuuliza maswali mengi, kwanini tuyapitie tunayopitia.
Ni ngumu sana mfano ukiwa na mgonjwa au ukiondokewa na mpendwa ukamshukuru Mungu. Hua tunajiuliza maswali mengi pasipo na majibu.

Ayubu alipitia wakati mgumu sana wa kuondokewa na watoto, mali zake zote mke, na kila alichokua nacho. Alifika wakati akasema, “Na ipotelee mbali ile siku niliyozaliwa mimi, Na ule usiku uliosema, Mtoto mume ametungishwa mimba.  Siku hiyo na iwe giza; Mungu asiiangalie toka juu, Wala mwanga usiiangazie”
Ayubu 3:3‭-‬4

Alilalamika kwa muda mrefu akilaumu kila kitu na kujibishana na marafiki zake. Akizungumzia jinsi alivyo mwenye haki mbele za Mungu.  Na Mungu alimsikiliza wakati wote huo. Akaamua kumjibu;  
Ayubu 38:1.. Mungu aliendelea kumuuliza Ayubu maswali mengi magumu.  Aliweka misingi ya ulimwengu, akaumba vyote vilivyopo, akatengeneza nyakati na misimu, na kila kitu in perfection.Akakuumba na wewe kwa namna ya ajabu kabisa lakini umesahau yote baada ya jaribu na kumtupia lawama. Baadae Mungu akasema: “Je! Mwenye hoja atashindana na Mwenyezi? Mwenye kujadiliana na Mungu, na ajibu yeye” (Ayubu 40:2)
Baada ya hapo Ayubu alijiona si kitu kabisa. Na akamwambia Mungu hana cha kujibu.

Ndiyo maisha tunayopitia hata sasa. Wakati Mungu anatutendea mambo mazuri tunafurahia na kumsifu Mungu sana. Lakini mambo yanapokua magumu tu tunaanza kuquestion ukuu wa Mungu na kujiuliza kama kweli Mungu anatusikia. Kutokuamini kunatufanya kuishi kwa wasiwasi kila mara.

Ni muhimu sana kujifunza kumshukuru Mungu kwa kila jambo. 1 Wathesakonike 5:18: “Shukuruni kwa kila jambo; maana hayo ni mapenzi ya Mungu kwenu katika Kristo Yesu”
Na ili uweze kufanya hivi ni kumruhusu yeye mwenyewe kukuwezesha. Kwa Mungu hakuna jambo lisilowezekana. (Wafilipi 4:13).

Ukishaweza kushukuru, Mungu atakuamini na kukupa mambo makubwa zaidi kwa sababu anajua imani yako ni thabiti.

Nini kinatufanya kusahau uwezo wa Mungu na kushindwa kushukuru?

  1. Adui
Shetani mara zote anataka uwe na wasiwasi na uwezo wa Mungu. Jaribu likija tu, anaanza kukuletea mawazo ya doubt uwezo wa Mungu, na njia mbadala za kutatua tatizo lako. Utawezaje kushinda? Maombi na kusoma neno. Fanya hivi kwa bidii. Usimpe shetani nafasi ya kukupa mawazo mabaya.

2. Watu
Tuwe makini na watu wanaotuzunguka. Wengine wakiona una tatizo wanaanza kukuletea njia tofauti na maombi kutatua tatizo lako. Kuna watu wana ushawishi mkubwa maishani mwetu. kama yupo anaekupa njia tofauti ya kufanikiwa, endelea kumheshimu lakini jaribu kumuepuka, na umuombee.

3. Changamoto nyinge za maisha.
Mfano, madeni, uchumi mdogo, ugomvi kwenye familia au ndoa n.k

Tunawezaje kushukuru wakati wa shida?

  1. Neno la Mungu.
Biblia ni njia sahihi ya mwongozo wa maisha yako. Jifunze kusoma neno kulishika na kuliishi kila wakati. Utaelewa uwezo wa Mungu vizuri, ahadi zake, na mipango yake kwenye maisha yako.
Mistari michache ya kujifunza kumshukuru Mungu: Waefeso 5:20, Zaburi 136:26, Zaburi 103:2, Wafilipi 4:4-7, Zaburi 23, 2 Petro 3:9.

2. Maombi
Ni muhimu sana kumwambia Bwana Yesu unachopitia, hata kama unajua anajua. Mkumbushe kila siku na kila wakati, popote ulipo. Ukiwa unatembea, kazini, nyumbani, shuleni, chagua mistari michache inayoshuhudia uwezo wa Mungu, ikariri na umkumbushe kua unajua alivyo mkuu na tatizo lako ni dogo tu, atalitatua. Fanya hivi  huku ukiamini kwa moyo kua anasikia na atajibu.

Ukiwa unamshukuru Mungu wakati wa majaribu, kwa njia ya kusoma na kuliamini neno lake, utagundua ahadi nyingi sana za Mungu kwako, ambazo ni kubwa kuliko tatizo lako. Ukizingatia ahadi hizi, zitakukumbusha uwezo wa Mungu wakati wote, kukusahaulisha tatizo lako, na utashinda jaribu na kusonga mbele.

Jambo la mwisho, Mungu hamjaribu binadamu. Mara nyingi watu hua wanasema, ni jaribu la Mungu. Yakobo 1:13 “Mtu ajaribiwapo, asiseme, Ninajaribiwa na Mungu; maana Mungu hawezi kujaribiwa na maovu, wala yeye mwenyewe hamjaribu mtu”

Majaribu yanatoka wapi, kwanini hata watu wenye imani thabiti hupitia majaribu.

Majaribu yanatoka kwa adui. Shetani hutengeneza bomu ili awapige wakristo. Ni kazi yake kujaribu kukuangusha. Kumbuka alivyomchochea Ayubu kwa Mungu.
Mungu hua anajua mpango wa adui lakini huyaruhusu majaribu yaje kwetu kama njia ya kuimarisha imani yetu.  Sala ya Bwana Yesu aliyotufundisha kwenye Mathayo 6, mstari wa 13 anasema  “usitutie majaribuni, lakini utuokoe na yule mwovu”. Maana yake Mungu kwa neema yake asimruhusu shetani atuletee majaribu. Lakini hata akiruhusu majaribu hayo yaje, 1 Cor 10:13, Mungu haruhusu jaribu linalozidi uwezo wetu. Kwa neema na uaminifu wake tunapata njia ya kutokea na tunashinda .
Usiogope majaribu, ukimtegemea Mungu na ukielewa mpango wake huna haja ya kuogopa. Yesu pia alijaribiwa na shetani, tena ana kwa ana, na alishinda.

Kwahiyo katika majaribu tuendelee kushukuru na kuamini kua Mungu ni mwaminifu na atatuokoa.
Imani yako inapimwa jinsi unavoihandle shida yako. Pamoja na kuomba Mungu akutoe katika jaribu linalokupata, ni muhimu zaidi kumshukuru kwa yale ambayo tayari amekupa. Ikiwemo uhai ulio nao hadi ukaweza kushuhudia jaribu hilo. 

No comments:

Post a Comment