Wednesday, 5 July 2017

Jinsi ya kuepuka wivu ili ufanikiwe


Bwana Yesu asifiwe!

Wivu ni jambo linalosumbua watu wengi. Watu wanasema kuna wivu wa aina mbili. Wivu wa maendeleo (kutaka kujifunza) na wivu mbaya wa kuchukia pale mtu mwingine  anapoendelea.
Habari ya wivu imeongelewa kwenye  Zaburi 73.

Katika jamii kuna mtu anaeweza jambo fulani kuliko mwingine, kimwili au kiroho, kwa sababu Mungu ametugawia karama mbali mbali tofauti. Kila mtu amepewa karama yake.

Yakobo na Esau, (Mwanzo 25: 21-34) Walianza kushindana toka tumboni mwa mama yao Rebeka (mst 22). Wote walikua wameandikiwa baraka,ya kua mataifa makubwa, lakini Mungu alisema watafarakana toka tumboni. 

Ndivyo ilivyo hata maisha ya sasa, kuna mashindano, kuna ambae ataonekana bora kwa jambo fulani kuliko mwingine. Lakini kila mtu ana kitu anachoweza kufanya.
 Tufanyaje ili tuweze kufanyia kazi uwezo wetu badala ya kuonea wivu wengine?



1. Maombi
Hii ni basic requirement. Huwezi kufanya jambo lolote hapa duniani bila msaada wa Mungu. Muombe akuwezeshe kuishi kwa kusudi alilokuwekea. Akuonyeshe ule uwezo na karama yako ili uvifanyie kazi.
2.  Imani thabiti
Moja ya sababu kubwa ya wivu ni kutoamini ahadi na mipango ya Mungu kwenye maisha yetu. Mwamini Mungu kwa moyo, bila kujali unapitia wakati gani. Usiamini nusu nusu, kwamba anaweza kukufanyia hiki na hiki hawezi.  Yeremia 29:11.  Mungu alishaweka misingi yako hapa duniani kabla hujazaliwa. Ukimwomba atakudhihirishia.
3. Usijifananishe na Mtu yoyote.  
Kila mtu ameumbwa kipekee kabisa. Zaburi 139:14. Ukifocus kuangalia maisha ya mwingine utapata woga, utashusha uwezo wako au utakata tamaa kwa sababu unaona yeye anafanya vizuri kuliko wewe. Ukishaamini wewe ni wa kipekee, mafanikio ya mwenzako hayatakupa shida. Usikubali kuchanganywa au kukatishwa tamaa. Kuna mifano mingi ya watu walioambiwa hawawezi na wakaweza. Na wewe unaweza. Ukishajua ile karama yako Mungu aliyokupa, fanya. Kwa uwezo wa Mungu lazima ufanikiwe.
“Lakini kila mtu na aipime kazi yake mwenyewe, ndipo atakapokuwa na sababu ya kujisifu ndani ya nafsi yake tu, wala si kwa mwenzake”
Wagalatia 6:4
4. Furahia mafanikio ya wengine!
Jifunze kufurahi pale rafiki na ndugu zako wanapofanikiwa.  Ukifanya hivo utamwonyesha Mungu kua unaamini mipango yake kwako.  Mungu ndio mtoa baraka, kwahiyo usiwe na wasiwasi. Kama amewakumbuka wengine atakukumbuka na wewe. Kua mvumilivu na mwaminifu kwa ahadi zake. Kama bado hujajua ufanye nini upate kuendelea, endelea kumkumbusha Mungu, atajibu siku moja.

Jambo la muhimu sana ni kuwa na imani. Imani inakufanya ujiamini kwa sababu unajua Mungu yupo upande wako.  Kama alisema hatakuacha, amini hatakuacha. Imani sio complicated unavyodhani, soma Biblia yako na amini ahadi za Mungu alizosema kwa ajili yetu. Lakini jambo la kwanza na muhimu zaidi ni kumwamininYesu kua Bwana na Mwokozi wa maisha yako, ili akupe imani ndani yako. Yohana 14:13-14.

No comments:

Post a Comment